Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Sa’īdī, khatibu wa swala ya Ijumaa ya tarehe 30 Aban (21/11/ 2025) iliyofanyika katika Muswala wa Quds mjini Qom Iran, sambamba na kutoa mkono wa pole kutokana na mnasaba wa siku za shahada ya Bibi Fatimah Zahraa (a.s), alieleza vipengele mbalimbali vinavyo husiana na utu wa Siddīqatul-Kubrā (a.s).
Imamu wa Ijumaa wa Qom, kwa kusisitiza nafasi isiyofanana ya maktaba ya Fātimiyya katika kuunda na kuendeleza harakati za kimungu, alibainisha kuwa maktaba hii ndiyo muundo mkuu wa malezi, uongofu na mfumo wa fikra wa harakati za wanaotafuta haki katika mtiririko wa historia na kwamba yamekuwa yakitoa hamasa ya uamsho kwa mataifa duniani.
Umuhimu wa utambulisho sahihi wa Bibi Zahraa (a.s)
Ayatullah Sa’īdī, akirejea msisitizo wa Ma’sumiin (a.s) juu ya kumtambulisha Bibi Zahraa (a.s) katika jamii kwa usahihi, alisema: Mtukufu huyu amekuwa mhimili wa matukio mengi yenye athari katika historia, na nafasi yake ya malezi katika kuunda mapinduzi ya Karbala ni nafasi ya msingi mno.
Maktaba ya Fātimiyya na Mapinduzi ya Karbala
Akaongeza kuwa: Iwapo leo tunazungumza kuhusu hamasa ya Karbala, ni lazima tufahamu kuwa wale waliopokea malezi ya maktaba ya Fātimiyya—yaani Imamu Husayn (a.s) na Bibi Zaynab (a.s)—ndio wabebaji wa ujumbe huo wa kimungu. Bila malezi ya Fātimiyya, mapinduzi ya Karbala yasingetokea, na harakati za kutafuta haki zisingeendelea katika historia.
Khatibu wa Ijumaa Qom, akirejea ilhamu ambayo harakati za ukombozi zimeipata kutoka Karbala, aliendelea kusema: Viongozi wakubwa kama Gandhi pia walijifunza somo la uhuru wa kweli na kupambana na dhulma kutoka katika mapinduzi ya Imamu Husayn (a.s), na ukweli huu ni muonekano ya mapinduzi ya Fātimiyya.
Daraja tukufu la Bibi Zahraa (a.s) katika riwaya
Ayatullah Sa’īdī, akitaja riwaya nyingi, alieleza nafasi maalumu ya Bibi Zahraa (a.s) na kusema: Kwa mujibu wa maneno ya Imamu Hassan al-Askari (a.s), Bibi Zahraa (a.s) ni hoja ya Mwenyezi Mungu juu ya mahujja wa Mwenyezi Mungu. Maana hii inaonesha kuwa; miaka 250 ya uimamu wa Ma’sumiin (a.s) ilizunguka kwenye mzunguko wa uongofu wa Bibi huyu mtukufu.
Akiashiria riwaya ya Shaykh Tūsī inayohusiana na maneno ya Imamu wa Zama (ajf), alisema: Uwepo mtukufu wa Waliyul-Asr (ajf) amemtambulisha Bibi Zahraa (a.s) kuwa ni kielelezo cha kudumu katika kipindi cha ghaiba na kudhihiri, na jambo hili linaonesha ukamilifu wa utu wake katika nyakati zote.
Imamu wa Ijumaa Qom, akiendelea, akarejea hadithi za Imamu Sadiq (a.s) kuhusu ukweli na utakaso wa Bibi Zahraa (a.s) na kuongeza: Kuwa Siddīqa kwa Mtukufu huyu kunamaanisha muafaka kamili wa fikra, maneno na matendo yake na ukweli wa kumuabudu Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo hakika ambayo imeuongoza mfululizo wa historia ya binadamu katika njia yake yenye nuru.
Ayatullah Sa’īdī, akirejea sehemu mojawapo ya ziara ya Bibi Zahraa (a.s), alisema: Mwenyezi Mungu anafahamu hadhi bora na daraja la majaribio alilolipitisha Bibi huyu, na daraja hili linaonesha ukubwa wa uwepo wake na nafasi yake katika njia ya uongofu wa wanadamu.
Akaendelea kusema: Katika riwaya, siku ya Kiyama, jeshi la Imamu wa Zama (ajf) limeelezwa kwa jina la “jeshi la Fātimiyya”, na jina hili linatokana na mtindo wa maisha ya Fātimiyya uliojengeka juu ya imani, ustahimilivu, akili na huruma.
Vipengele vya Mapinduzi ya Fātimiyya: Nguvu ya ndani na huruma
Imamu wa Ijumaa Qom, katika kufafanua vipengele vya mapinduzi ya Fātimiyya, alisema: Sifa ya kwanza ya harakati hii ni uwezo wa ndani na wa kiroho; uwezo unaotokana na fitra ya kimungu, ambao haushindiki na una athari, tofauti na nguvu za kijuujuu za kibeberu ambazo mwishowe huangamia.
Akaongeza kuwa: Malezi ya kistratejia ya Bibi Zahraa (a.s) ni mfano wa wazi wa nguvu hii ya ndani, na wasichana na wanawake katika jamii kwa kuiga mfano huo wanaweza kupata kinga dhidi ya mashambulizi ya kiutamaduni na kuwa na athari chanya katika jamii.
Imamu wa Ijumaa Qom alieleza kuwa sifa ya pili ya harakati ya Fātimiyya ni huruma na mapenzi kwa wanadamu, na akasisitiza: Mwenendo wa Mtume (s.a.w) na Bibi Zahraa (a.s) ulikuwa ni udhihirisho wa mapenzi ya kimungu, na roho hii ndiyo iliyoasisi misingi mingi ya maadili na thamani katika kijamii.
Maoni yako